Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kuwa inatambua umuhimu wa kujenga vituo vya polisi nchi nzima ili kutoa huduma ya ulinzi kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Daniel Baran Sillo, ameyaeleza hayo Bungeni jijini Dodoma, alipokua akitolea ufafanuzi swali la mbunge wa viti maalum, Mh. Mwatum Dau Haji, aliyeuliza, kuna mpango gani wa kuongeza kasi ya ujenzi wa vituo vya Polisi nchini.

Akitoa majibu hayo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Sillo ameliambia Bunge kuwa utekelezaji wa mpangon wa ujenzi unategemea fedha zinazotengwa toka kwenye bajeti ya Serikali kila mwaka, kutoka kwenye mfuko wa Tuzo na Tozo pamoja na michango ya kujitolea ya wananchi na wadau mbalimbali.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa, Naibu Waziri Mh. Sillo amelitaarifu Bunge kuwa, Serikali imeshajenga vituo vya Polisi daraja A, B, C 487 na vituo vidogo vya kata/shehia 667 nchini.

Akiendelea kuonyesha azma ya Serikali ya kuongeza kasi ya ujenzi wa vituo vya Polisi, Mh. Sillo amesema kasi ya Serikali ya awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendana na upatikanaji wa fedha.