Wiki iliyopita, Rais Samia alihutubia kongamano la wanahabari ambapo alipokea pia mukhtasari wa ripoti kuhusu hali ya kiuchumi kwenye vyombo vya habari nchini. Pamoja na mengine, katika hotuba yake Rais alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari nchini kufanya uchambuzi wa habari kitaalamu. Alibainisha kuwa kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa uchambuzi wa kina katika upashaji wa habari nchini.
“Nasikiliza sana habari, lakini uchambuzi ni kidogo sana. Mnafanya 'reporting' kuliko 'analysis',” alisema Rais Samia, akimaanisha kwamba vyombo vingi vya habari nchini vinaelekea zaidi kutoa taarifa bila uchambuzi wa kina unaoweza kuleta tija zaidi kwa jamii.
Changamoto Zinazosababisha Ukosefu wa Uchambuzi wa Habari
Kwa uzoefu wangu, Kuna mambo kadhaa yanayochangia changamoto hii, na ni muhimu wadau wa habari na vyombo vya habari kuchukua hatua za kuongeza tija katika upashaji wa habari;
1. Elimu na Utaalamu wa Wanahabari
Wanahabari wengi hujifunza taaluma ya habari bila kuwa na msisitizo katika eneo makhususi la kitaalamu. Hali hii inasababisha waandishi kuandika na kuripoti aina mbalimbali za maudhui bila kuwa na eneo maalum la ubobezi. Ni vigumu kwa mwanadamu kujua kila kitu, hivyo si rahisi kwa mwanahabari kujua masuala ya kijamii, sheria, uchumi, au michezo kwa undani wote. Hii ndiyo sababu waandishi wengi huishia kuripoti tu bila uchambuzi wa kina.
2. Uhuru wa Habari na Hofu ya Kiuandishi
Mazingira ya uhuru wa habari kihistoria yametingisha ustawi wa uandishi wa kina. Waandishi wengi huogopa kugusa maudhui nyeti kama ya kisiasa au kiuchumi kwa undani. Hii imejenga hofu miongoni mwa waandishi, hata kama wana weledi katika maudhui hayo, hivyo wanachagua kuripoti juu juu tu.
3. Ukosefu wa Wanataaluma katika Vyombo vya Habari
Ni nadra kwa vyombo vya habari kuajiri wanataaluma katika fani husika kama wachumi, watafiti, au wanasheria kwa ajili ya uchambuzi wa taarifa. Badala yake, wanategemea wageni kwenye vipindi vya programu mbalimbali ambao hufanya kazi hizo bila malipo, hali inayopunguza uwezo wa ufikishaji wa habari kwa undani.
Mapendekezo ya Kuboresha Uchambuzi wa Habari
Ili kuboresha hali hii, vyombo vya habari vinapaswa kuchukua hatua kadhaa muhimu:
1. Kuimarisha Uandishi wa Ubobezi
Vyombo vya habari vinapaswa kuhamasisha uandishi wa ubobezi kwa kuwapa waandishi maeneo maalum ili waweze kufuatilia, kujisomea, kudadisi, na kupata mafunzo rasmi katika fani hizo. Kwa mfano, mwandishi wa habari za takwimu anaweza kujiunga na programu za kitaaluma kuhusu takwimu, uchumi, na uchambuzi wa data ili kuongeza weledi wake.
2. Kuajiri Wanataaluma
Vyombo vya habari vinapaswa kuajiri na kushirikiana na wanataaluma kama wanasheria, wachumi, na wahasibu ili kusaidia kutengeneza maudhui, kufanya uchambuzi, na kuhariri taarifa. Makubaliano maalum ya kunufaisha pande zote yanapaswa kuwekwa ili kuhakikisha kazi hizi hazifanywi bure.
3. Kushirikiana na Waandishi Huru
Vyombo vya habari vinaweza kushirikiana na waandishi huru (freelance writers) ambao wamejielekeza katika maeneo maalum. Hii inaweza kusaidia vyombo vinavyokosa rasilimali watu katika maeneo Fulani kumudu kupata maudhui na kuboresha ufikishaji wa habari zake.