Na; Rashid Aziz
Dar es Salaam - Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 imewasilishwa jana mbele ya Bunge na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 49.37 katika matumizi ya kawaida na ya kimaendeleo kwa mwaka ujao wa fedha. Hii ni ongezeko la asilimia 10 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana ya shilingi trilioni 44.38.
Miongoni mwa yaliyowasilishwa katika mapendekezo ya bajeti ni hatua za kibajeti zinazogusa sekta ya sukari. Pendekezo la kwanza ni kubadili sheria ya sukari ili kuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua na kuratibu pengo la sukari.
Pili, ni marekebisho kwenye kanuni ya NFRA yanayolenga kuifanya sukari kuwa bidhaa muhimu kwa usalama wa chakula.
Kwa tafsiri yetu, hatua hizi zitamaanisha kuwa NFRA sasa itakuwa na uwezo wa kununua au kuagiza sukari, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo waagizaji waliopewa vibali ndio waliokuwa wakiagiza bidhaa hiyo.
Sukari imeingizwa katika orodha ya bidhaa muhimu kwenye hifadhi ya chakula ya taifa, hivyo NFRA itakuwa na jukumu la kutunza bidhaa hiyo katika hifadhi yake kama ilivyo kwa bidhaa nyingine muhimu.
Ingawa hatua hizi zinaweza kuleta manufaa, changamoto ya msingi ya uzalishaji usiotosheleza wa sukari kwa wazalishaji wa ndani itaendelea kuwepo. Viwanda vya sukari vya ndani vinazalisha wastani wa tani 300,000 tu kwa mwaka, wakati mahitaji ya nchi ya sukari kwa matumizi ya kawaida na viwandani yanakadiriwa kufikia tani 655,000 kwa mwaka (Wizara ya Kilimo, 2021).
Bajeti ingeweza kuleta tija nzuri zaidi kama hatua zake zingelenga kupunguza gharama za uzalishaji sukari kwenye viwanda vya ndani, kuwezesha sekta ya kilimo cha miwa, au kuchukua hatua za kupunguza gharama za malighafi zinazotumika kuzalisha sukari.
Hatua hizi zingesaidia kukuza uzalishaji wa ndani wa sukari, kudhibiti bei, na kupunguza utegemezi wa bidhaa hiyo kutoka nje, na kwa kiasi fulani ingesaidia kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa hiyo.
Kwa sasa, hatua za kibajeti zitasaidia kupunguza makali ya uhaba wa sukari usiotabirika, ingawa suluhisho la muda mrefu na madhubuti bado linahitajika.