Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa hamasa kubwa ya kuongeza kasi ya ukuaji wa kiuchumi, tokea alipopokea kijiti cha kuiongoza Tanzania.

Mageuzi makubwa yanayoshuhudiwa sasa yametokana na msingi wa kisera wa Serikali ya awamu ya Sita, yaliyoegemea zaidi katika diplomasia ya uchumi kama namna kuu ya kufikia na kutimiza malengo ya kitaifa, kupitia mahusiano na mataifa mengine na washirika wa maendeleo wasio mataifa.

Diplomasia ya uchumi kwa tafsiri ya Mh. Dkt. Samia, inajikita katika kuufungua uchumi wetu kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuboresha miundombinu na huduma za jamii, kuboresha mifumo ya kikodi, na kuonyesha ubora wa Tanzania kwa ulimwengu mzima kupitia maonesho ya kimataifa.

Uwanda huu wa maonesho, ambao hapo awali ulikuwa unafanywa kwa ukawaida, sasa umepewa msukumo maalum na wa kipekee, kama namna ya kuchochea muingiliano kati ya wafanyabiashara wa ndani na wa nje.

Maonesho ya kibiashara ya Dar es salaam ya sabasaba na yale ya Wakulima ya nanenae, yamebadilishwa taswira na Serikali ya awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuwa diplomasia ya maonesho inayotumika kufanikisha malengo mahsusi ya kitaifa ya kuinua na kukuza uchumi, kupitia rasilimali na fursa mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Takwimu za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini, zinaonyesha kuwa zaidi ya wafanyabiashara 3,840 wameshiriki maonesho ya mwaka huu wa 2024. Muingiliano huo unaohusisha wafanyabiashara kutoka Ulaya, Asia na Amerika, unatafsirika kama diplomasia ya maonesho ambao kwa aina yake unarahisisha kuifanya Tanzania kivutio cha uwekezaji kwa kutoa fursa kubwa kupitia kuruhusu wafanyabiashara kuonyesha bidhaa na biashara zao, na kuwapa nafasi ya kujionea bidhaa za wafanyabiashara wengine wa maeneo mbalimbali.

Kutokana na kuwa maonesho ya sabasaba na nanenane ndio makubwa zaidi na yenye mvuto mkubwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, yanafuzu kujulikana kama aina ya diplomasia ya maonesho ambalo ni zao la diplomasia ya uchumi inayotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kutokana na msukumo wa kuinua uwezo wa kiuchumi wa watanzania anaoufanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni wazi watanzania wapo kwenye kipindi kizuri zaidi kujiendeleza kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kumuunga mkono Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na kutoa mitaji pamoja na kubuni sera wezeshi za kupunguza urasimu na kuhamasisha ushiriki wa kimkakati wa wananchi wa Tanzania.