Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga jumla ya nyumba 860 za walimu wa msingi na sekondari nchini katika jitihada za kuongeza ufanisi wa walimu na kuwapunguzia gharama za maisha.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mh. Zainab Katimba ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Namtumbo Mh. Vita Kawawa aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa nyumba za walimu wa sekondari nchini na kukarabati zilizochakaa.
Naibu Waziri Katimba ameliambia bunge kuwa Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya upungufu wa nyumba za walimu wa msingi na sekondari ambayo inatakiwa kutatuliwa.
Mh. Katimba amesema kuwa katika mwaka 2022/23 na mwaka 2023/24, Serikali kupitia fedha za progaramu za kuimarisha elimu ya awali na msingi imejenga nyumba 860 za walimu wa shule za msingi na sekondari zitakazokuwa na uwezo wa kubeba jumla ya familia 2,018.
Akiendelea kuonyesha msisitizo na dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita, chini ya uongozi unaojali wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha mazingira ya walimu, Mh. Zainab Katimba amelieleza bunge kuwa katika mwaka 2024/25 Serikali itajenga jumla ya nyumba 562 zitakazokuwa na uwezo wa kuchukua familia 1,124.
Naibu Waziri, Zainab Katimba pia amelihakikishia bunge kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutenga fedha kupitia programu za miradi mbalimbali na Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu, ili walimu wapate mahali bora pa kuishi.